Isaiah 51:1-6

Wokovu Wa Milele Kwa Sayuni


1 a“Nisikilizeni, ninyi mnaofuatia haki
na mnaomtafuta Bwana:
Tazameni mwamba ambako mlichongwa,
na mahali pa kuvunjia mawe ambako mlichimbwa;

2 bmwangalieni Ibrahimu, baba yenu,
na Sara, ambaye aliwazaa.
Wakati nilipomwita alikuwa mmoja tu,
nami nikambariki na kumfanya kuwa wengi.

3 cHakika Bwana ataifariji Sayuni,
naye atayaangalia kwa huruma magofu yake yote;
atayafanya majangwa yake yawe kama Edeni,
nazo sehemu zake zisizolimika ziwe kama bustani ya Bwana.
Shangwe na furaha zitakuwako ndani yake,
shukrani na sauti za kuimba.


4 d“Nisikilizeni, watu wangu;
nisikieni, taifa langu:
Sheria itatoka kwangu;
haki yangu itakuwa nuru kwa mataifa.

5 eHaki yangu inakaribia mbio,
wokovu wangu unakuja,
nao mkono wangu utaleta hukumu kwa mataifa.
Visiwa vitanitegemea
na kungojea mkono wangu kwa matumaini.

6 fInueni macho yenu mbinguni,
mkaitazame dunia chini;
mbingu zitatoweka kama moshi,
dunia itachakaa kama vazi,
na wakazi wake kufa kama mainzi.
Bali wokovu wangu utadumu milele,
haki yangu haitakoma kamwe.

Copyright information for SwhKC